UISLAMU NI DINI YA MANABII WOTE

 

Qur’ani inathibitisha kwamba nyumati zote katika zama mbali mbali walipelekewa Mitume waliowafundisha wao Dini ya Allah Mtukufu, na Mtume Muhammad amani iwe juu yake ameelezwa ndani ya Qur’ani ;

 

إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ بِالْحَقِّ بَشِيرًا وَنَذِيرًا ۚ وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ }   سورة فاطر:24}

 

“Hakika Sisi Tumekutuma wewe kwa Haki, kuwa ni mbashiri na mwonyaji. Na hapana umma wowote ila ulipata mwonyaji kati yao.” (Q35:24)

Mitume wote walikuja na Dini ya haki na wao hawatofautiani katika ujumbe wa Imani na misingi ya hukumu na tabia.
Na Uislamu aliokuja nao Mtume wa mwisho, Muhammad - Swallallaahu alayhi wasallama kabla ya miaka zaidi ya elfu moja na mia nne ni mwendelezo wa Dini waliyokuja nayo wale Mitume waliyomtangulia; na Qur’ani inawaamrisha waislamu waamini yale waliyotumwa nayo wale Mitume waliopita kama vile Nabii Ibrahim-Alayhi salaam, Nabii Is-haqa-Alayhi salaam, Nabii Yakobo-Alayhi salaam, na Nabii Isa- Alayhi salaam;

 

قُولُوا آمَنَّا بِاللَّهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْنَا وَمَا أُنزِلَ إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَمَا أُوتِيَ النَّبِيُّونَ مِن رَّبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ              سورة البقرة:136

 

“Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu Kwake.” (Q2:136)

Na katika yenye kutia mkazo ni kuwa Qur’ani imetusimulia sisi usia wa Nabii Ibrahimu-Alayhi salaam, baba wa manabii, kwa wanawe, na mfano wake ni Nabii Ya’aquub kwa wanawe wakati alipokaribia kufariki duniya kwa kuwaambia - hakika Allah Mtukufu Amekuchagulieni nyinyi Dini ya haki kuweni imara katika Uislamu mpaka mtakapofikiwa na kifo;

 

 وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ}    سورة البقرة:132}

 

“Na Ibrahim akawausia wanawe, na pia Yaaqub: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu Amekuteulieni Dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu, wanyenyekevu.” (Q2:132)

Kwa ushahidi huu Dini hii ni mwendelezo wa Dini ya Manabii wote. Itikadi ni moja haibadiliki katika asili yake, bali mabadiliko ni katika sharia na upambanuzi wa hukumu kwa kwenda sawa na hali za zama mbali mbali, mpaka alipotumilizwa duniyani Mjumbe wa mwisho aliye Mtukufu wa daraja Mtume Muhammad - Swallallaahu alayhi wasallama, ili aweke sharia ya mwisho kwa watu wote.

Na hapa Qur’ani inathibitisha kwa uwazi kuwa dini ni moja nayo ni Uislamu, na kuwa hizi tofauti tunazozishuhudia kati ya watu wenye kufuata dini zilizotoka mbinguni katika upande wa itikadi, hapana ila ni upotoshaji ndio uliowaweka wao mbali na yale waliyokuja nayo Mitume wao.

 

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّهِ الْإِسْلَامُ ۗ وَمَا اخْتَلَفَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ ۗ وَمَن يَكْفُرْ بِآيَاتِ اللَّهِ فَإِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ }   سورة آل عمران:19

 

“Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa Kuhisabu.” (Q3:19)