Malezi ni msingi wa jamii yeyote.Jamii ikitaka kupiga hatua na kuwa na maendeleo ni sharti izingatie malezi bora.Pasi na malezi mazuri yenye lengo na shabaha hakutakuwa na maendeleo,kwa hivyo kuna dharura kubwa sana ya jamii kuzingatia suala la malezi.Kuna haja ya sisi kulea watoto na nafsi zetu katika misingi ya sawa.Ndio tunapata katika Qur’an imeanza na tazkiya ya nafsi ya ndani inayoletwa na malezi mazuri.Katika Suratul Jumuah,aya ya pili,ALLAH (SWT) ameanza na tazkiya ya kusafisha dhamira ya ndani ambayo ni kazi ya tarbia kisha ikatajwa elimu na hekima.

 

{هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ}

 

[Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.] [Al-Jumu":2]

Kwa sababu hii ni wazi kuwa malezi ndio muhimu.
Kama hujui malengo ya kumlea mtoto wako basi ufahamu uko katika hasara kubwa sana.

Malengo ya ulezi hayaanzi baada ya kuzaa mtoto bali pale ulipoanza kufikiria kutafuta baba au mama wa watoto wako.Hapo ndipo palipoanzia malengo ya ulezi.Hii ni kwa sababu athari za wazazi wawili ni muhimu sana katika malezi ya watoto.